Na Jabali Media
Spika wa Bunge la taifa Moses Masika Wetang’ula, ametoa msaada wa shilingi milioni 2 kupiga jeki shughuli za klabu ya Nzoia Sugar.
Nzoa Sugar inayoshiriki ligi ya daraja la pili (NSL), awali iligonga vichwa vya habari kutokana na matatizo ya kifedha.
“Nimekabidhi shilingi milioni 2 kwa uongozi wa Nzoia Sugar kusaidia kushughulikia changamoto za kiutendaji zinazokumba timu hiyo, ili kuhakikisha inakamilisha msimu huu kwa mafanikio,” alitangaza Spika Wetang’ula.
Spika ambaye ni shabiki shakiki wa timu hiyo, alimtia moyo mwenyekiti Evans Kadenge na uongozi wake, akiwataka kuendeleza juhudi za kuimarisha timu kupitia mafunzo na kuendeleza ustadi wa wachezaji.
Kwa upande wake, Kadenge alishukuru kwa mchango huo akisema kuwa ni msaada mkubwa katika kukabiliana na changamoto zinazoikumba klabu hiyo.
“Spika, tunashukuru kwa msaada wako wa mara kwa mara. Tunaahidi kuwa tutaendelea kutia bidii na kujituma kwa maendeleo na ustawi wa klabu,” alisema Kadenge.
Mbunge wa Kanduyi John Makali, alimpongeza Kadenge kwa juhudi zake za kuongoza klabu hiyo, akisisitiza kuwa vijana wana vipaji ambavyo klabu zinapaswa kugundua na kukuza, hasa wakati wa likizo ndefu.
Naye Seneta wa Bungoma David Wafula Wakoli, aliwahimiza vijana kujitahidi kushiriki michezo, akisema ni sekta yenye manufaa makubwa kifedha.