10
Sun, Nov

Hakikisho la rais Ruto kuhusu maandalizi ya AFCON 2027

Rais wa CAF na rais wa Kenya. Picha/Ikulu

Tools
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Jabali Media

Rais William Samoei Ruto amewahakikishia Wakenya na Waafrika kwa ujumla, kwamba Kenya itakuwa tayari kuandaa dimba la taifa bingwa barani Afrika (AFCON), mwaka 2027.

Makala hayo ya 36 yataandaliwa kwa pamoja na Kenya, Uganda na Tanzania.

Akizungumza alipokutana na rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) dakta Patrice Motsepe katika Ikulu ya rais jijini Nairobi hii leo, Ruto amesema kuwa ukarabati wa viwanja vya Nyayo na Kasarani unaendelea vyema, sambamba na ujenzi wa uga mpya wa Talanta Sports.

“Nakuhakikishia kuwa viwanja vya Nyayo na Kasarani vitakuwa tayari mwishoni mwa mwaka huu ili kuandaa mechi za kipute cha wachezaji wanaoshiriki ligi za nyumbani (CHAN) mwaka ujao, huku ujenzi wa uga wa Talanta ukikamilika mwezi Disemba mwaka ujao ili kuandaa mtanange wa AFCON mwaka 2027,” alisema rais Ruto.

Hapo jana, dakta Patrice Motsepe alizuru viwanja hivyo akiandamana na Waziri wa michezo Onesimus Kipchumba Murkomen, na rais wa Shirikisho la soka nchini (FKF) Nick Mwendwa miongoni mwa wengine.

Rais huyo wa CAF alieleza kuridhishwa na kasi inayoendelea ya ukarabati na ujenzi katika viwanja hivyo.

“Nina hakika kwamba tukishirikiana vyema, Kenya itakuwa tayari kuandaa michuano hiyo,” alisema rais huyo wa CAF.

Daktari Motsepe vile vile anatarjiwa kuzuru Uganda na Tanzania, ili kuweka kwenye mizani maandalizi ya mataifa hayo ya Afrika Mashariki, katika kuandaa michuano ya AFCON.