Na Leonard Murunga
Mbunge wa Embakasi Mashariki Paul Ongili almaarufu Babu Owino, ameelezea sababu ya kutofika bungeni hapo jana, wakati wa kikao cha kujadili na kupigia kura hoja ya kumtimua naibu wa rais Geoffery Rigathi Gachagua.
Kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X, mbunge huyo amesema kuwa hapakuwa na haja yake kujadili kuondolewa mamlakani kwa naibu wa rais, wakati akiwa na maswala mengine muhimu ya kushughulikia.
Amesisitiza kuwa angehudhuria kikao hicho, iwapo maswala muhimu kama vile pendekezo la Kampuni ya Adani kupewa kandarasi ya kusimamia uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kanyatta (JKIA) kwa kipindi cha miaka 30, mfumo mpya wa kufadhili elimu ya vyuo vikuu, bima ya afya ya jamii (SHA), ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana, gharama ya juu ya maisha na ushuru wa juu unaotozwa wananchi, yangeshughulikiwa.
"Mtaniona bungeni ikiwa masuala hayo yatawasilishwa lakini ukweli ni kwamba hawatayaleta. Nilikuwa nimeshughulika sana na mambo mengine muhimu na ya dharura yanayowahusu wapiga kura wangu,” akasema Owino.
“Kasi ambayo wabunge walitumia kumtimua Rigathi pia inapaswa kuwa ile ile inayotumika kutatua changamoto zinazowakumba wakenya,” akaongeza mbunge huyo anayehudumu kwa muhula wa pili.
Wabunge 281 walipiga kura ya kuunga mkono hoja ya kuondolewa mamlakani kwa Gachagua, 44 wakapinga, huku mmoja akikosa kupigia kura hoja hiyo iliyowasilishwa bungeni na mbunge wa Kibwezi Magharibi, Eckomas Mwengi Mutuse.
Wabunge kwenye kikao cha kumtimua Rigathi Gachagua. Picha/Hisani
Mutuse aliwasilisha mashtaka 11 dhidi ya Rigathi Gachagua, akidai hafai kushikilia wadhifa wa naibu wa rais. Gachagua alikanusha tuhuma hizo, wakati alipojitokeza bungeni kujitetea.
Babu pamoja na mwenzake wa Kiharu Samson Ndindi Nyoro hawakuwepo bungeni wakati wa mchakato wa kumtimua Gachagua, huku maswali yakiibuliwa kuwahusu.
Macho sasa yanaelekezwa kwa bunge la Seneti, ambapo kikao cha maseneta wote kitaamua hatima ya Gachagua wiki ijayo.
Hii ni baada ya maseneta leo asubuhi kukataa pendekezo la kubuni kamati maalum ya maseneta 11, kuchunguza mashtaka dhidi ya Gachagua.
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Babu Owino ‘afunguka’ kuhusu sababu ya kususia kikao cha kumtimua Gachagua
Typography
- Smaller Small Medium Big Bigger
- Default Helvetica Segoe Georgia Times
- Reading Mode