Wana-ODM Kisumu washabikia Nyong’o kupewa mikoba ya Raila

Viongozi wa ODM wakiwahutubia wanahabari jijini Kisumu mnamo Ijumaa. Picha/Hisani FB

Politics
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Jabali Media

Viongozi na wanachama wa ODM katika kaunti ya Kisumu, wameelezea furaha mpwito mpwito, baada ya gavana wa Kisumu Profesa Peter Anyang’ Nyong’o kuteuliwa kaimu kinara wa chama hicho cha chungwa.

Siku ya Jumatano, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alitangaza uteuzi wa Nyong’o kuwa kaimu kinara wa chama hicho, huku Odinga akijitosa rasmi kwenye kampeini za Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa bara Afrika (AUC).

Uchaguzi utaandaliwa mwezi Februari mwakani jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, ambapo Odinga anamenyana na wapinzani watatu katika harakati za kumrithi Moussa Faki Mahamat, ambaye mda wake wa kuhudumu unaendelea kuyoyoma.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Kisumu hii leo, viongozi na wanachama wa ODM kutoka maeneo bunge yote saba ya kaunti hiyo ya Ziwa wakiongozwa na mwenyekiti Paul Akeyo, wamempongeza Odinga kwa kuidhinisha uteuzi wa Nyong’o.

Akeyo amesema kuwa kama Katibu Mkuu mwanzishili wa chama cha ODM, Nyong’o ana kila kigezo cha uongozi kumsaidia kusukuma gurudumu la chama hicho kikubwa cha upinzani nchini, wakati Odinga akiwinda kiti cha AUC.

“Wanachama wa ODM katika kaunti ya Kisumu siku zote wamekuwa na imani kwa Nyong’o kutokana na ueledi wake katika uongozi,” alisema Akeyo.

Nyong’o alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa chama cha ODM mwaka 2005, ambapo alihudumu kama Katibu Mkuu mwanzilihi.

Akeyo amesema kuwa Nyong’o amechangia pakubwa katika kukua na kuimarika kwa chama hicho, tangu mwaka 2005.

Kwa upande wake, naibu gavana wa Kisumu Mathews Ochieng Owili amesema kuwa wataendelea kuwaunga mkono kwa dhati Odinga na Nyong’o, akisisitiza kuwa ije mvua au lije jua, Odinga atasalia kinara wa ODM.

ODISH2.jpg

Viongozi na wanachama wa ODM katika kaunti ya Kisumu baada ya kuwahutubia wanahabari Ijumaa. Picha/Hisani FB

“Tunamtakia Odinga kila la heri. Tunajua marais barani Afrika watampigia kura ili awe mwenyekiti wa AUC. Hata akichaguliwa, Odinga atasalia kinara wa ODM kwa njia moja au nyingine,” akasema Owili.

Kauli yao imeungwa mkono na mbunge wa Kisumu ya Kati dakta Joshua Odongo Oron, na Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti ya Kisumu Ruth Odinga, walio-ongeza kuwa ni mapema mno kusherehekea ‘ushindi wa Odinga AUC.’

“Raila Odinga bado hajachaguliwa mwenyekiti wa AUC, tafadhali tuache sherehe za mapema,” akaonya Bi. Odinga.

“Hizi kauli za giniwasekao (hiki kitu tushachukua) lazima zikome. Tuendelee kumuombea Raila ili achaguliwe mwenyekiti wa AUC,” akasisitiza Oron.

Kwa upande wake, kiranja wa wengi katika bunge la kaunti ya Kisumu, aliyepia Mwakilishi wa Wadi ya Markert Milimani Seth Ochieng Kanga almaarufu Adui Nyang,’ ameshikilia kuwa Odinga atasalia kinara wa ODM hata akichaguliwa mwenyekiti wa AUC.

“Baba (Raila) bado ni Baba hata akiwa Addis Ababa, hata akiwa Johannesburg, hata akiwa Ouagadougou, bado ni Baba.”