Babu Owino avunja kimya chake kufuatia kuzuiliwa nchini Tanzania

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino. Picha/Hisani

National Politics
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Collins Wambulwa

Mbunge wa Embakasi Mashariki Paul Ongili almaarufu Babu Owino, anamtaka rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kuwafafanulia wakenya sababu kuu iliyoifanya serikali yake kumzuilia mwezi Disemba mwaka jana.

Mbunge huyo anadai kuzuiliwa kwa muda wa saa tatu kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, kisha baadaye akaruhusiwa kurudi Kenya bila ya kukamilisha ziara yake nchini humo.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, Owino amemkashifu rais Suluhu, akisema kuwa wakenya humkaribisha kila wakati akija humu nchini, lakini mbunge wa Kenya anapofanya ziara katika nchi yake, anakabiliana na vizingiti.

“Rais wa Tanzania anafaa kuwafafanulia watu wa Embakasi Mashariki, Jamhuri ya Kenya na wakenya, sababu iliyoifanya serikali yake kunizuilia kwa saa tatu kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Akija Kenya, sisi humkaribisha kama rafiki, lakini mbunge aliye uongozini anapozuru Tanzania, anahangaishwa. Hilo halikuabaliki,” aliandika Owino.

Amesema kuwa maafisa wa uhamiaji wa Tanzania walimtia mbaroni kwa kisingizio cha kutokuwa na idhini ya kuingia nchini humo, licha ya kuwa na stakabadhi hitajika za usafiri.

“Nilishangazwa sana kwa yale niliyofanyiwa. Hakuna ufafanuzi faafu uliotolewa kufuatia kunyimwa ruhusa ya kuingia Tanzania. Kama kiongozi na mwananchi mfuata sheria, hicho kitendo hakikubaliki,” aliongeza Owino.

Kupitia waraka aliyoundamanisha kwenye mtandao wake wa facebook, ambao pia aliutuma kwa serikali ya Tanzania kutaka kujua sababu ya kuzuiliwa kwake, na kumtaka rais wa Tanzania kumjibu pia kupitia barua, mbunge huyo alisikitikia hali hiyo na kuitaja kuwa ya ukandamizamizaji.

Mbunge huyo amevunja kimya chake, siku chache baada ya raia wa Tanzania kwa jina Maria Sarungi Tsehai, ambaye ni mwanaharakati na mhariri kwenye shirika moja la habari nchini Tanzania, kutekwa nyara katika eneo la Chaka karibu na mtaa wa Kilimani jijini Nairobi mwezi jana.  

Tsehai alikuwa ameenda kusukwa nywele katika eneo la Chaka, kabla ya wanaume watatu waliokuwa kwenye gari aina ya Toyota Noah kumteka nyara.

Hata hivyo, aliachiliwa baadaye jioni kufuatia kuingilia kati kwa mashirika mbalimbali ya kutetea haki za kibinadamu, kama vile Chama Cha Wanasheria Nchini (LSK) na shirika la Amnesty International tawi la Kenya.

Mwanaharakati huyo ni mkosoaji mkuu wa rais wa Tanzania.