By Jabali Media
Baadhi ya wakazi wa Gem kaunti ya Siaya na Luanda kaunti ya Vihiga wamepinga mradi wa uchimbaji dhahabu wa Ramula-Mwibona.
Mradi huo unaofahamika kama ‘Open Pit Mining,’ umependekezwa na kampuni ya Shanta Gold.
Chini ya vuguvugu la Concerned Citizens, wakazi hao wakiongozwa na Profesa Fred Ogolla, wamesema kuwa mradi huo utasababisha madhara mengi kuliko manufaa ikiwa utaruhusiwa kuendelea.
Kama wakazi wa eneo hilo, wamesema kwamba hawapingi shughuli za uchimbaji wa dhahabu kuendeshwa na kampuni yoyote eneo hilo, ila wanachopinga ni kile kinachoonekana kuwa ukosefu wa uwazi katika oparesheni za kampuni ya Shanta Gold.
Ogolla amesema kwamba wakazi wa eneo hilo wanaishi kwa hofu ya kuhamishwa kutoka ardhi za mababu wao, akiongeza kuwa hakuna kiwango chochote cha fedha kinachoweza kufidia hali ya watu kuondolewa kwenye ardhi ya jadi.
“Wakazi wa Ramula kupitia ombi kwenye bunge la kaunti ya Siaya, waliibua maswali muhimu kuhusu mradi huo huku wakielezea pingamizi zao,” akasema Profesa Ogolla.
Kulingana naye, maafisa wa kampuni hiyo hawajachukua nafasi kusemezana na wakazi kuhusu mradi huo, akidai kuwa walifahamishwa kupitia ripoti ya Mamlaka ya utunzi wa mazingira nchini (NEMA), kwamba ardhi yao itachukuliwa kwa min-ajili ya kufanikisha mradi huo wenye utata.
“Hilo kamwe halikubaliki,” akasema.
Wameitaka kampuni hiyo kusikiliza maoni yao na kusitisha shughuli, pamoja na kuweka wazi haki za uchimbaji migodi walizonazo katika eneo hilo, miongoni mwa matakwa mengine.
Wametishia kuwasilisha kesi kortini katika kipindi cha siku saba zijazo, ikiwa lalama zao hazitashughulikiwa.
Mkazi Amunge Silaba ameikosoa kampuni hiyo kwa kukosa kupeana wananchi fursa ya kutoa maoni yao kuhusu mradi huo.
“Walipokuja, hawakutuita kwenye kikao ili tutoe maoni yetu,” akasema.
Kampuni ya Shanta Gold huendesha shughuli zake katika nchi za Kenya na Tanzania.
Mradi wa uchimbaji dhahabu wa Ramula-Mwibona wapata pingamizi
Tools
Typography
- Smaller Small Medium Big Bigger
- Default Helvetica Segoe Georgia Times
- Reading Mode