Serikali za kaunti zatakiwa kuwajibikia tiba ya sumu ya nyoka

Mkurugenzi wa Shirika la Acccess to Medicines Platform Dorothy Okemo. Picha/LM

News
Tools
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Leonard Murunga

Serikali za kaunti zimetakiwa kutenga fedha za kununua dawa za kukabili makali ya sumu ya nyoka, kama njia ya kuokoa maisha ya wanaoumwa na wanyama hao.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutoa uhamasisho kuhusu kuumwa na nyoka katika eneo bunge la Shinyalu kaunti ya Kakamega juma hili, mkurugenzi wa shirika la Access to Medicines Platform Dorothy Okemo, alisema kuwa pana haja ya kuhakikisha kuwa hospitali zote za mashinani zina dawa za kuwatibu wanaoumwa na nyoka.

“Tunazirai serikali za kaunti hasa maeneo yaliyo na nyoka wengi kutenga fedha ili hospitali zote za mashinani ziwe na dawa za kuwasaidia waathiriwa,” alisema Okemo.

Aidha, amependekeza kuwa wanafunzi watumike kama mabalozi wa kutoa uhamasisho kuhusu kuepuka kuumwa na nyoka katika jamii.

“Mbinu ya kusambaza ujumbe huu ili ufikie watu wengi ni kutumia wanafunzi ambao kuelewa kwao ni haraka mno.”

Kwa upande wake, Catherine Shiechi ambaye ni msimamizi wa huduma za afya katika kaunti ndogo ya Shinyalu, amesema kuwa kuna changamoto ya kuweka dawa za kushughulikia waathiriwa wa mashambulizi ya nyoka kwenye vituo vya afya vya kiwango cha chini, kwa sababu ya gharama yake ya juu.

Amewahimiza wakaazi wawe makini wanapofanya shughuli zao ili kuepuka kuumwa na nyoka, akishauri yeyote atakayeumwa kutafuta matibabu haraka iwezekanavyo.

“Dawa hizi ni vigumu kuhifadhiwa katika vituo vyetu vya afya kwa sababu ya gharama. Kila mmoja anafaa kuchukua tahadhari ili kuzuia kuumwa na nyoka. Waathiriwa wanafaaa kutafuta huduma za matibabu haraka iwezekanavyo,” aliongeza afisa huyo wa afya.

Naye Raydon Imbwaka ambaye ni afisa wa afya ya jamii, ametoa wito kwa wakazi kukata nyasi karibu na makaazi yao, ili kuzuia uvamizi wa nyoka.

Florence Ludeki, mwalimu mkuu was shule ya msingi ya Chirobani kwa upande wake alipongeza uhamamisho huo, aliosema uliwafumbua macho kuhusu hatua za kuzuia kuumwa na nyoka, kauli iliyoungwa mkono na baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo.

Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutoa uhamasisho kuhusu kuumwa na nyoka huandaliwa kila Septemba 19. Takwimu zinaonesha kuwa takribani watu 20,000 huumwa na nyoka humu nchini kila mwaka. 4,000 kati yao hufariki.