Mgomo walemaza shughuli za usafiri JKIA

Wasafiri wakwama JKIA. Picha/Hisani FB

News
Tools
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Ellon Odhiambo

Mgomo wa wafanyakazi wa viwanja vya ndege, umelemaza shughuli za kawaida katika viwanja mbali mbali vya ndege nchini.

Mgomo huo umeathiri pakubwa shughuli katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, uwanja wa kimataifa wa Moi (MIA) jijini Mombasa na uwanja wa kimataifa wa Kisumu (KIA) jijini Kisumu, huku kampuni za ndege kama vile Kenya Airways na Jambojet zikifutilia mbali baadhi ya safari.

Hali hiyo, ilisababisha mamia ya wasafari kukwama kwenye viwanja vya ndege. 

Wafanyakazi wanaogoma wanapinga mchakato wa kampuni ya Adani ya India, kuchukua usimamizi wa uwanja wa JKIA, kwenye mkataba utakaodumu miaka 30.

Kampuni ya Adani inapanga kukodesha uwanja wa JKIA kwa kima cha dola billioni 1.85.

Wakosoaji wanasema kuwa mkataba huo utasababisha ukosefu wa ajira, na kuwaongezea walipa ushuru mzigo wa madeni.

Juma hili, maafisa wa chama cha mawakili nchini (LSK) na tume ya kutetea haki za binadamu nchini (KNCHR), walipata agizo la mahakama kusitisha kwa mda mchakato wa kampuni ya Adani kusimamia uwanja wa JKIA.

JKIA ni miongoni mwa viwanja vikubwa vya ndege barani Afrika. Uwanja huo uliwahudumia takribani abiria millioni 8.8, huku ukipitisha tani 380,000 za mizigo kati ya mwaka wa 2022 na 2023.

Hata hivyo, umekumbwa na ukusefu wa umeme pamoja na paa zinazovuja wakati mvua inaponyesha. Kampuni ya Adani inapanga kujenga njia ya kurukia ndege, na kuboresha miundo msingi kwenye uwanja huo.

Maamlaka ya viwanja vya ndege nchini (KAA) kwenye taarifa imeutaja mgomo huo kama usio halali, huku katibu mkuu wa muuungano wa kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini (COTU-K) Francis Atwoli, akimnyoshea kidole cha lawama aliyekuwa waziri wa barabara na uchukuzi Kipchumba Murkomen, kwa matatizo yanayoshuhudiwa JKIA kwa sasa.