Na Zuleikha Salim
Bunge la kaunti ya Uasin Gishu hii leo linampiga msasa Evans Kapkea, ambaye ni naibu wa gavana mteule.
Anapigwa msasa na wanachama wa kamati ya uteuzi, kwenye bunge hilo.
Ikiwa ataidhinishwa na bunge la kaunti, Kapkea mwenye umri wa miaka 34, ataziba pengo la mhandisi John Barorot aliyejiuzulu Agosti 21, miaka miwili baada ya kuchaguliwa pamoja na gavana Jonathan Bii, almaarufu Koti Moja.
Barorot alijiuzulu baada ya kuteuliwa afisa mkuu mtendaji kwenye kampuni moja ya kimataifa kuhusu Habari, Mawasiliano na Teknologia.
Hadi uteuzi wake hivi maajuzi, Kapkea amekuwa mwakilishi wa Wadi ya Tembelio, na mwanachama wa kamati mbali mbali kwenye bunge la kaunti ya Uasin Gishu.
Baadhi ya wawakilishi wa Wadi za kaunti ya Uasin Gishu, wameapa kuidhinisha uteuzi wake, kutokana na kile wanachosema ni desturi yake ya uchapa kazi.