Na Collins Wambulwa
Aliyekuwa seneta wa Kakamega Cleophas Malala amevunja kimya chake, baada ya kuachiliwa huru kutokana na kukamatwa kwake Jumatano usiku, kwa kutunga mchezo ‘tata’ wa kuigiza wa “Echoes of War.”
Mchezo huo ulifaa kuigizwa na wanafunzi wa shule ya wasichana ya Butere katika tamasha za kitaifa za michezo ya kuigiza na filamu, zinazoendelea jijini Nakuru.
Amesimulia hali aliyopitia kabla ya kuachiliwa huru, akisema kuwa baada ya kukamatwa, alipelekwa kwenye kituo cha polisi cha Nakuru.
Baada ya kipindi kifupi, alitiwa kwenye buti ya gari aina ya Subaru na kupelekwa hadi mahali pasipojulikana. Hatimaye aliachiliwa leo mchana bila ya kuandikiwa kosa lolote.
“Nilikamatwa na kuwekwa kwenye buti ya gari aina ya Subaru, kisha nikapelekwa msituni na maafisa wa DCI. Baadaye walinifikisha katika kituo cha polisi cha Nakuru, halafu wakanipeleka Eldama Ravine ambako walinifunga hata bila kunipa maji, chakula au kuniruhusu kuonana na mawakili wangu. Ni saa chache zilizopita tu ndipo wameniachilia bila kuniandikia kosa lolote,” alisimulia Malala, ambaye ni mwandani wa aliyekuwa naibu wa rais, Rigathi Gachagua.
Katibu huyo mkuu wa zamani wa cahama tawala cha UDA, ameelezea kusikitishwa kwake akisema kuwa kufikia sasa, ameandika michezo 82 ya kuigiza ikiwemo ule wa “Shackles of Doom,” ambao pia ulikabiliwa na hali tata ya kufungiwa, chini ya utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Katika mchezo wa “Echoes of War,” Malala aliangazia masaibu kama vile changamoto zinazozingira bima mpya ya afya nchini (SHA), namna ya kuimarisha uongozi nchini kwa kuishi kwenye mazingira yasiyofungamana na ufisadi, mfumo mpya wa elimu (CBC) na changamoto zinazokumba ufadhili wa elimu ya wanafunzi wa vyuo vikuu.
“Mchezo huu unaangazia masuala ya vijana wa Gen Z, ambao wanataka nchi yao iwe na bima ya afya ambayo inafanya kazi,” aliongeza seneta huyo wa zamani.
Ameilaumu serikali ya rais William Ruto kwa kile anachosema ni jitihada za ‘kuwazimia taa’ viongozi jasiri ambao wanafichua uozo serikalini.
“Mimi ningependa kuwaomba mawakili wangu, fanyeni lolote linalowezekana ili mhakikishe mchezo huo umefanikishwa. Rudini mahakamani na mpate amri ya hao watoto kuigiza kabla ya hadhira,” akasema Malala.
Aidha, ameitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati kwa kuwa ‘haki za watoto,’ zimeingiliwa hasa kwa kuwanyimwa haki yao ya kuigiza kwenye tamasha za kitaifa.