Wevarsity Sacco yailambisha sakafu Water Project mjini Kakamega

Viongozi wa Wevarsity Sacco wakisalmiana na wachezaji. Picha/LM

Tools
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Leonard Murunga

Timu ya kandanda ya Wevarsity Sacco ndio mabingwa wa makala ya mwaka huu ya kipute cha Akiba Derby, baada ya kuichabanga Water Project goli moja kwa nunge, kwenye fainali iliyogaragazwa katika uga wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknologia cha Masinde Muliro (MMUST) mjini Kakamega, hapo jana.

Bao la ushindi lilifungwa katika kipindi cha kwanza, huku wana-Wevarsity Sacco wakituzwa kombe maridadi kufuatia ushindi huo.

Kwenye mechi ya kutafuta mshindi wa tatu, KUDHEIHA ilipepeta Bodaboda mabao 2 kwa nunge katika mtanange wa kusisimua.

Akizungumza baada ya ushindi huo, kocha wa Wevarsity Sacco Wellington Oyombe ambaye pia anahudumu kama kocha wa Kakamega Rangers, alisema kuwa mashindano yalikuwa ya kupigiwa mfano, kutokana na ushindani mkali ulioshuhudiwa.

“Wapinzani walikuwa wamejipanga vyema hivyo kufanya mashindano kuwa uwanja wa kujifundisha. Kama kocha, nitarekebisha makosa ya hapa na pale yaliyojitokeza wakati wa michuano,” akaongeza kocha Oyombe.

Eric Wagaka, afisa wa timu ya Water Project alisema kuwa licha ya kupoteza kwenye fainali, wachezaji hawakuondoka mikono mitupu, kwani walipata fursa ya kipekee ya kujiimarisha kiafya, kupitia kushiriki mshindano hayo.

“Tunahitaji kulinda afya zetu ili kuitumikia jamii kwa ukakamavu zaidi,” alisema afisa huyo.

Kauli yake ilitiliwa mkazo na kocha mkuu wa Water Project, Wycliffe Nyando Kereda.

“Tumefika fainali ila hatukushinda. Tumekuwa na mchezo mzuri,” alisema kocha huyo.

WE1.jpg

Wachezaji wa Wevarsity na Water Project kabla ya kuanza kwa mechi ya fainali. Picha/LM

Mashindano hayo ya siku nne yaling’oa nanga siku ya Jumanne, chini ya ufadhili wa chama cha Ushirika cha WeVarsity huku timu mbali mbali zikigombania taji la kandanda na neti boli.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Wevarsity Sacco Chrisandus Wanjala Nakitare, amesema kuwa kwa mda mrefu, wanachama wa chama hicho cha ushirika wamekuwa wafanyakazi wa chuo kikuu cha MMUST, ila sasa wamefungua milango yao kwa mkenya yeyote aliye na nia ya kujiunga nao.

Amesema kuwa huduma zao sasa zinapatikana katika kaunti za Vihiga, Kakamega, Bungoma, Busia na Trans Nzoia.

“Tulilenga kupitisha ujumbe kuhusu Wevarsity Sacco na ninaamini kwamba lengo hilo limeafikiwa, kwa sababu watu wamekuja kwa wingi.”

This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.