15
Tue, Oct

Kocha wa Spurs akiri wana kibarua dhidi ya Arsenal

Kocha wa Spurs Ange Postecoglou. Picha/Hisani FB

Tools
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Jabali Media

Kocha mkuu wa Tottenham Hotspur Ange Postecoglou, amekiri kwamba vijana wake watakabiliwa na mlima telezi wa kukwea, watakapopambana na washika bunduki Arsenal kwenye mtanange wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza (EPL) hapo kesho.

Spurs itakuwa mwenyeji wa Arsenal ugani Tottenham Hotspur Stadium kuanzia saa kumi alasiri hapo kesho, kwenye debi ya kwanza ya London msimu huu.   

Akizungumzia mechi hiyo, Postecoglou amesema kuwa wachezaji wa Arsenal wamekuwa pamoja kwa mda mrefu chini ya meneja Mikel Arteta, akiongeza kuwa itakuwa mechi ya ‘kufa mtu’ kwa timu zote mbili.

“Hawajabadilisha timu yao pakubwa sana. Umoja wao umewabeba sana kwenye misimu miwili iliyopita ambapo walimaliza nafasi ya pili nyuma ya Manchester City,” alisema kocha huyo raia wa Australia.  

“Wanajiamini sana, na hilo bila shaka linawasaidia kujenga msingi imara wa kupambana kwa ajili ya kushinda taji la ligi,” akaongeza.

Hata hivyo, Kocha huyo amesema kuwa mechi ya kesho inatoa nafasi bora kwa vijana wake kushinda ili kutawala London Kaskazini.

Postecoglou alijiunga na Spurs msimu jana, na rekodi yake ya ukufunzi inaashiria kuwa huanza kushinda mataji kwenye msimu wake wa pili.

Alijiunga na Spurs kutokea miamba wa soka nchini Scotland, Celtic, alikoshinda mataji mawili ya ligi kwa mpigo, kati ya mwaka 2021 na 2023.

AR1.jpg

Wachezaji wa Arsenal wakiwa mazoezini. Picha/Hisani FB

Huenda sajili mpya wa Arsenal, Riccardo Calafiori na Mikel Merino pamoja na nahodha Martin Odegaard wakakosa mechi hiyo, kutokana na majeraha.

Kiungo Declan Rice atakuwa nje akihudumia marufuku, baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya Brighton majuma mawili yaliyopita.

Kocha Arteta anatarajiwa kumhusisha pakubwa wing’aa Raheem Starling, aliyejiunga na Arsenal akitokea Chelsea, japo kwa mkopo wa msimu mmoja.

“Ninachoona kwake ni mchezaji aliye na kiu cha kutaka kucheza kila dakika ya mechi. Ikiwa hilo halifanyiki, basi anakosa furaha. Anapenda kandanda,” akasema Arteta kumhusu Sterling.

Sio mara ya kwanza kwa Arteta kushirikiana na Sterling. Wawili hao walifanya kazi pamoja kwa miaka mitatu, kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 wakati Arteta alipokuwa naibu wa kocha, katika klabu ya Manchester City.

Arsenal ni ya 4 ligini kwa alama 7 baada ya kushinda mechi 2 na kutoka sare 1 msimu huu, huku Spurs ikishikilia nafasi ya 11 kwa alama 4, baada ya ushindi kwenye mechi 1, sare 1 na kupoteza mechi 1 dhidi ya Newcastle United.