15
Tue, Oct

Hatuogopi Cameroon, kocha Firat ‘achemka’ baada ya ushindi dhidi ya Namibia

Kocha wa Harambee Stars Engin Firat. Picha/Hisani

Tools
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Jabali Media

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka Harambee Stars Engin Firat, amewataka wachezaji wa timu ya taifa ya soka ya Cameroon almaarufu Indomitable Lions, kuanza kutayarisha vichwa vyao ili kunyolewa kwa ‘wembe bila maji.’  

Kenya na Cameroon zitakutana kati kati ya mwezi ujao wa Oktoba, kwenye mechi mbili za kundi J kuwania kufuzu kipute cha taifa bingwa barani Afrika (AFCON) makala ya mwaka ujao nchini Morocco.

Kwenye kikao na wanahabari baada ya Harambee Stars kuinyuka Namibia mabao 2 kwa 1 ugani Orlando, jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini jana usiku, Firat alisema kuwa Cameroon inafaa kujiandaa kwa mechi za kufa kupona dhidi ya Harambee Stars.

“Cameroon wanafaa kuanza kufikiria kuhusu jinsi ya kutushinda. Hatuogopi Cameroon,” akasema Firat.

Aidha, kocha huyo raia wa Uturuki amelalamikia kile anachosema ni kukosa uungwaji mkono wa mashabiki wa Kenya, akiwaponda kwa umaarufu wa kukosoa bila kutoa suluhu wala kujitokeza uwanjani kuishabikia timu.

Kocha huyo amesema kuwa licha ya kuiweka Kenya kwenye mkondo wa kufuzu AFCON kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2019, hajalipwa mshahara wake na shirikisho la soka nchini (FKF) kwa miezi 9.  

Akizungumza baada ya ushindi dhidi ya Namibia, nahodha wa Harambee Stars beki Joseph Okumu alisema kuwa watapambana kiume, hadi wapate tiketi ya kuelekea Morocco.

Baada ya mechi dhidi ya Cameroon mwezi ujao, Harambee Stars itachuana na Zimbabwe ugenini, kisha Namibia nyumbani kwenye mechi mbili za mwisho za makundi mwezi Novemba.

Timu za kwanza mbili kwenye kundi hilo, zitafuzu dimba la AFCON mwaka 2025. Kenya inaongoza kundi hilo kwa alama 4 baada ya sare dhidi ya Zimbabwe na ushindi dhidi ya Namibia.

Cameroon ni ya pili kwa alama nne, ila inadunishwa kwa ubora wa mabao baada ya ushindi dhidi ya Namibia na sare dhidi ya Zimbabwe.