15
Tue, Oct

Makala ya tatu ya kipute cha gavana Barasa kuzinduliwa mwishoni mwa mwezi huu

Tools
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Jabali Media

Timu mbali mbali za kandanda na raga, zinaendelea kupasha misuli moto kwa makala ya tatu ya kipute cha gavana wa Kakamega Fernandes Odinga Barasa.

Kulingana na ratiba tuliyo nayo, uzinduzi utafanyika tarehe 28 mwezi huu, kabla ya nyasi kuanza kuumia na nguo kuchanika kwenye nyuga mbali mbali, katika maeneo bunge yote 12 ya kaunti hiyo.

Maeneo bunge hayo ni Butere, Mumias Magharibi, Matungu, Likuyani, Mumias Mashariki, Khwisero, Shinyalu, Lurambi, Ikolomani, Lugari, Malava and Navakholo.  

Mechi za kiwango cha Wadi zitagaragazwa kati ya Septemba 28 na Novemba 2, kabla ya wakali wao kukutana kwenye kiwango cha maeneo bunge kuanzia Novemba 23 hadi Disemba 18, ili kuamua timu zitakazomenyana kwenye mechi za muondoano, raundi ya 16 bora, robo fainali na kisha semi fainali kati ya Disemba 29 na Disemba 31.

Mechi za kutafuta mshindi wa tatu na kisha fainali kwa akina dada na wanaume zitasakatwa Januari Mosi mwaka ujao, ili kutambua mabingwa wapya wa kaunti.

Kindumbwendumbwe cha raga kitaandaliwa kati ya Disemba 27 na 28 mwaka huu.

Gavana Barasa alianzisha michuano hiyo mwaka 2022 baada ya kuchaguliwa, ili kukuza vipaji vya vijana katika kaunti hiyo, ambayo ni maarufu kwa talanta za kandanda na raga.

Umri FC walitawazwa mabingwa upande wa wanaume kwenye makala ya kwanza ya dimba hilo kwa kuichabanga Arsenal Lirhembe 2-1 katika fainali, kabla ya Young Simba kutwaa taji la makala ya pili kwa ushindi wa goli moja kwa nunge, dhidi ya Maroon Commandoes.