Chama cha ODM kitaongoza taifa – Nyong’o

Kaimu kinara wa ODM Anyang' Nyong'o akihutubia wanahabari Jumanne. Picha/Hisani

Politics
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Jabali Media

Kaimu kinara wa chama cha ODM Anyang’ Nyong’o, ameelezea matumaini ya chama hicho cha chungwa kuongoza taifa siku za usoni.

Akizungumza katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kisumu (KIA) Jumanne adhuhuri, alikowasili kwa mara ya kwanza tangu kupokezwa rasmi wadhifa wa kaimu kinara wa ODM mwishoni mwa juma, Nyong’o amesema kwamba chama hicho kimepitia pandashuka nyingi tangu kuundwa mwaka 2005, akiongeza kwamba uwezekano wa kuunda serikali ni mkubwa mno.

“Katika chama hiki, hakuna nafasi ya ubinafsi. Msiogope, tushirikiane kukijenga chama hiki ambacho kinaelekea kuongoza taifa hili. Tunaweza kuona kizazi baada ya kizazi kikija tayari kuongoza nchi hii,” akasema gavana huyo wa Kisumu.  

Nyong’o anaziba pengo la kinara wa chama cha ODM Raila Odinga, japo kwa mda.

Odinga tayari ametoa makucha kuwinda kiti cha Mwenyekiti wa Tume ya Bara Afrika (AUC), huku uchaguzi ukipangwa kuandaliwa mwezi Februari mwakani, jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Waziri huyo Mkuu wa zamani anamenyana na wapinzani wanne, ambao ni Anil Gayan wa Mauritius, Richard Randriamandrato wa Madagascar na Mahamoud Ali Youssouf wa Djibouti.

Wachambuzi wanasema kuwa farasi ni wawili - Ali Youssouf na Odinga.

Nyong’o amemshukuru Odinga kwa kumuamini kiwango cha kumuachia usimamizi wa ODM, wakati akijotosa rasmi kwenye kampein za wadhifa wa AUC.

Amewarai viongozi na wafuasi wa chama hicho, kumuunga mkono kwa dhati ili afanikiwe katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.

“Najua mkiniunga mkono, nitatoshea kwenye vyatu hivi vikubwa nilivyopewa kuvalia,” akaongeza Nyong’o.

KSM2.jpg

Gavana wa Kisumu Anyang' Nyong'o akisindikizwa na wafuasi wa ODM katika uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kisumu mnamo Jumanne. Picha/Hisani

Naye mwenyekiti wa chama hicho, aliyepia gavana wa kaunti ya Homabay Gladys Wanga, amesema kwamba hawana budi ila kufuata nyayo za Odinga, hasa kipindi hiki anapocheza ‘ligi ya bara Afrika.’

“Unajua mahali chama kimetoka na changamoto ambazo tumepitia. Tunaamini na hatuogopi kusema kuwa chama kitafauli chini ya uongozi wako.”

Kando na Wanga, wengine waliokuwa kwenye uwanja huo kumlaki Nyong’o ni pamoja na gavana wa Migori George Ochillo Ayacko, mbunge wa Kisumu Magharibi Rosah Akinyi Buyu, mbunge wa Nyando Jared Okello, mbunge wa Seme James Nyikal, mbunge wa Kisumu ya Kati Joshua Oron na mbunge wa Nyakach Aduma Owuor, miongoni mwa wengine.

Msafara wa Nyong’o kisha ulifululiza moja kwa moja hadi nyumbani kwao eneo la Ratta, Seme, kwenye ibada ya shukrani.

Waandishi: Florence Omollo na Johnson Juma.