15
Tue, Oct

Notisi ya hoja ya kumbandua Gachagua yawasilishwa bungeni

Naibu wa rais Rigathi Gachagua. Picha/Hisani

Politics
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Zuleikha Salim

Notisi ya hoja ya kumbandua mamlakani naibu wa rais Geoffrey Rigathi Gachagua almaarufu Riggy G, imewasilishwa kwenye bunge la kitaifa, hii leo.

Hoja hiyo imewasilishwa bungeni na mbunge wa Kibwezi Magharibi Eckomas Mutuse Mwengi, aliyesema kuwa hana chuki ya aina yoyote dhidi ya nabibu wa rais.

Mbunge huyo ameelezea bunge kwamba wakati mwafaka, atadhibitisha kila dai lililo kwenye hoja hiyo dhidi ya Gachagua.

Mutuse aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Maendeleo Chap Chap (MCCP) chake waziri wa Leba Alfred Mutua, alisoma orodha ya majina ya wabunge wote 291 waliotia sahihi hoja ya kumbandua Gachagua ofisini. 

Mwishoni mwa juma, kiongozi wa wengi bungeni aliyepia mbunge wa Kikuyu Anthony Kimani Ichung’wah, alidhibitisha kuwa hoja hiyo ingewasilishwa bungeni, akiongeza kuwa atakuwa miongoni mwa watakaopiga kura kuidhinisha kutimuliwa kwa Gachagua.

Kimani anamshutumu Gachagua kwa kuendeleza siasa za kikabila, badala ya kuchapa kazi, hivyo basi kuyumbisha jitihada za serikali ya Kenya Kwanza kufanikisha mchakato wa maendeleo nchini.

Gachagua anadaiwa kukiuka kifungu cha 10 cha Katiba, ambacho kinaangazia maadili na kanuni za uongozi.

Kiongozi huyo anakabiliwa na tuhuma za uchochezi, kando na kukiuka vifungu vya 147, 148, 174, 186 na 189 vya Katiba, vinavyozungumzia mwenendo na wajibu wake kama msaidizi wa rais William Ruto.

Aidha, anabanwa na tuhuma za kujipatia mali kwa njia ya ufisadi. Mali hiyo inasemekana kusambazwa katika kaunti za Nyeri, Nairobi na Kilifi.

Ikiwa wabunge watapistisha hoja ya kumtimua, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Masika Wetang’ula atawasilisha azimio hilo kwa Spika wa bunge la Seneti Amason Jeffa Kingi, ndani ya siku mbili, ili maseneta waamue mstakabali wake kwenye serikali ya Kenya Kwanza.

Gachagua ameonya kuwa rais Ruto atakabiliwa na mlima telezi wa kupanda wakati wa kuomba kura mwaka 2027 katika eneo la Mlima Kenya, ikiwa hoja ya kumtimua afisini itaidhinishwa na mabunge yote mawili.

“Ninataka kumsihi Rais Ruto aiweke sawa nyumba yake na aturuhusu kufanya kazi. Tuna jukumu la kutimiza kwa wakenya,” alisema Gachagua hivi maajuzi.

Kiongozi huyo sasa anakabiliwa na hatari ya kuwa naibu wa rais wa kwanza kutimuliwa afisini kupitia hoja ya kutokuwa na imani naye, chini ya Katiba ya sasa iliyorasimishwa mwaka 2010.

This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.