Siwezi kubali kuajiriwa na Ruto, asema Seneta Onyonka

Seneta wa Kisii Richard Onyonka. Picha/Hisani FB

Politics
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Ellon Odhiambo 

Seneta wa kaunti ya Kisii Richard Onyonka amesema kuwa hana nia ya kuajiriwa na serikali, kutokana na hali kwamba huenda rais Willliam Ruto asipendezwe na baadhi ya kauli zake.  

Onyonka akijibu swali kuhusu uwezekano wa kuhajiriwa kwenye serikali ya Kenya Kwanza, alisema, “siwezi kwa sababu rais hatapenda maneno yangu.’’

Seneta huyu aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, amesisitiza kuwa atasalia kwenye upinzani.

Ni miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa utawala wa Ruto, akipinga pakubwa mfumo mpya wa kufadhili elimu ya wanafunzi wa vyuo vikuu, akiutaja kama unaoendeleza ubaguzi. 

Aidha, Onyonka amesema kwamba japo kinara wa ODM anaunga mkono serikali ya Kenya Kwanza, ataendelea kutekeleza majukumu yake kama Seneta.

Kauli ya Seneta huyo imejiri kufuatia hatua ya rais Ruto, kuwateua vigogo wanne wa chama cha ODM, kwenye baraza lake la mawaziri.

Wanne hao ni Ali Hassan Joho (Waziri wa Madini na Uchumi Samawati), Wycliffe Oparanya (Waziri wa Vyama vya Ushirika), James Opiyo Wandayi (Waziri wa Kawi) na John Mbadi (Waziri wa Fedha).

Hadi uteuzi wao mwezi Juni, Joho na Oparanya walikuwa manaibu vinara wa chama cha ODM, Mbadi alikuwa mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho cha chungwa, ilihali Wandayi alikuwa kiongozi wa wachache katika bunge la taifa.