15
Tue, Oct

Tumieni vitabu vilivyoidhinishwa, wasimamizi wa shule za kibinafsi wahimizwa

Afisa Mkuu Mtendaji wa KICD Charles Ong'ondo akiwahutubia wanahabari jijini Kisumu. Photo/LM

News
Tools
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Leonard Murunga

Wasimamizi wa shule za kibinafsi wamehimizwa kuhakikisha kuwa wanafunzi na walimu kwenye shule zao, wanatumia vitabu vilivyoidhinishwa na Taasisi ya Maendeleo ya Mtaala nchini (KICD).

Akizungumza baada ya kongamano lililowaleta pamoja wanachama wa muungano wa shule za kibinafsi nchini (KEPSA) jijini Kisumu mnamo Alhamisi, afisa mkuu mtendaji wa KICD Profesa Charles Ochieng Ong’ondo, alisema kuwa shule za kibinafsi zimepiga hatua kubwa katika kuisaidia serikali kutekeleza mtaala mpya wa elimu nchini, almaarufu CBC.

“Shule za kibinafsi hutekeleza jukumu kubwa katika kutimiza maono ya serikali kwenye sekta ya elimu, hasa kwenye mtaala mpya wa CBC. Nafurahi kwamba shule hizo zinaongoza katika jitihada za kuimarika kwa sekta ya elimu nchini,” alisema Ong’ondo.

Hata hivyo, afisa huyo amewahimiza wasimamizi wa shule hizo kununua vitabu vilivyoidhinishwa na KICD, huku akiwarai wazazi kuwa msitari wa mbele katika kufanikisha elimu ya wanao.

“Mnavyojua ni kwamba tuna mtaala mpya. Ikiwa unataka kununua vitabu au vifaa vya masomo, tafadhali wasiliana nasi ili upate vitabu sahihi.”  

Kwa upande wake, Rosemary Birenge ambaye ni mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Kisumu, alisisitiza kuwa serikali kuu inashirikiana na shule za kibinafsi, ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata fursa sawa za elimu.

“Wanafunzi wote, walio kwenye shule za umma au za kibinafsi ni wetu. Lazima tuendelea kushirikiana ili kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata fursa sawa ya masomo,” akasema Birenge.

Naye Charles Ochome, Mwenyekiti wa KEPSA aliyepia Mkurungenzi wa shule za Golden Elites jijini Kisumu, amesema kwamba shule za kibinafsi zinaendelea vyema na utekelezaji wa mtaala wa CBC.