15
Tue, Oct

Dawa ya deni ni kulipa, wakenya wakumbushwa

Waziri wa vyama vya ushirika Wycliffe Oparanya. Picha/Jabali Media

News
Tools
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Jabali Media

Waziri wa vyama vya ushirika Wycliffe Ambetsa Oparanya, amewakumbusha wakenya kuhusu umuhimu wa kulipa deni baada ya kukopa.

Akizungumza wakati alipofunga rasmi warsha ya siku tatu ya wanachama wa bodi ya Hazina ya Uwezo kwenye hoteli moja jijini Kisumu hii leo, Oparanya amesema kuwa wanaokopa fedha za umma wanafaa kulipa kwa wakati, ili wakenya wengine wanufaike.

Oparanya amepuuzilia mbali madai kwamba Hazina kama vile ‘Uwezo Fund,’ ‘Husler Fund’ na ‘Youth Fund’ miongoni mwa nyingine zilibuniwa kisiasa, ‘hivyo wanaokopa wanafaa kustarehe tu bila kulipa.'

Aidha, ametoa changamoto kwa wasimamizi wa hazina za umma kuwa wabunifu, katika jihudi za kuhakikisha kuwa wanapata fedha za kuendesha oparesheni zao.

“Lazima muwe wabunifu, mambo yanabadilika. Sharti muanze kufikiri kuhusu jinsi ya kupata pesa za kuendesha oparesheni zenu. Mgao wa wizara ya fedha unaendelea kudidimia kila uchao,” akaonya gavana huyo wa zamani wa Kakamega.

Amegusia wazo la kutoza riba ya chini kama vile asilimia mbili, kama mojawepo ya hatua za kimkakati.

Vile vile, gavana huyo amesema tayari amepokea pendekezo la kuunganisha hazina zote za serikali, ila akaongeza kuwa uamuzi wa kisiasa unahitajika, kabla ya kutolewa kwa mwelekeo mwafaka.

Naye Susan Auma Mang’eni, katibu katika wizara hiyo amesema kwamba tayari wamepeana mikopo ya shilingi bilioni 57 kwa wakenya kupitia Hazina ya Halsa, tangu ianzishwe takribani miaka miwili iliyopita.

Kulingana naye, wakenya milioni 46 wamenufaika, huku kiwango cha kulipia mikopo kikiwa asilimia 79. Amewahimiza wakenya kukopa na kulipa kwa wakati, kauli iliyoungwa mkono na Ann Njuguna, mwenyekiti wa bodi ya Hazina ya Uwezo.