10
Sun, Nov

‘Nitawashtaki kwa Raila,’ Ruto awaambia wakazi wa Kondele

Rais Ruto akiwahutubia wakazi wa Kondele. Photo/Courtesy FB

News
Tools
Typography
  • Smaller Small Medium Big Bigger
  • Default Helvetica Segoe Georgia Times

Na Jabali Media

Rais William Samoei Ruto, ametishia ‘kuwashtaki’ wakazi wa eneo la Kondele jijini Kisumu kwa kinara wa chama cha ODM Raila Odinga, ikiwa wataendelea ‘kumsumbua.’

Akiwahutubia wakazi wa Kondele mnamo Jumamosi kwa mara ya kwanza tangu alipolazimika kuondoka eneo hilo kwa kasi ya farasi wakati msafara wake uliposhambuliwa kwa mawe mwaka 2021, wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, Ruto amesema kuwa wana-Kondele wamekuwa mwiba kwenye kidole chake kwa muda mrefu.

Wakati huo, Ruto alikuwa naibu wa rais akipasha misuli moto kumenyana na Odinga kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2022, ambapo aliibuka mshindi.

"Watu wa Kondele, kumbe ni nyinyi? Niko na kesi kubwa na nyinyi watu wa Kondele. Mmenitesa sana,” alisema Ruto mnamo Jumamosi.

Amesema kuwa ikiwa ‘usumbufu' wa wana-Kondele hautakoma, hatakuwa na budi ila kuwashtaki kwa Baba (Raila Odinga).

“Mkiendelea kunitesa nitawashtaki kwa Baba na mkizidi nitawashtaki kwa Mungu.”

Amewapongeza waakazi hao kwa kumkaribisha kwa vifijo, shangwe, nderemo na hoi hoi, kinyume na ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita.

“Wacha nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa kunikaribisha hapa Kisumu pacho,” akasema kiongozi wa nchi.

Ruto alianza ziara yake katika eneo la Nyanza mnamo Jumatano, ambapo alizuru Kaunti za Migori, Homabay na Siaya kabla ya kutua Kisumu kwa uzinduzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo.

Alifunga safari ya Nyanza siku moja baada ya kuongoza hafla ya uzinduzi wa mchakato wa Odinga, kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Bara Afrika (AUC).

Uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa AUC, kuziba pengo la raia wa Chad Moussa Faki Mahamat anayeondoka, utaandaliwa mwezi Februari mwaka ujao, jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Odinga anamenyana na wapinzani watatu, akilenga kuwa mkenya wa kwanza kutwaa wadhifa huo.